6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWEKA DIRA YA KUJENGA MIJI YA KISASA, SALAMA NA ENDELEVU

 
Na Munir Shemweta, WANMM.

Tanzania inatarajiwa kuwa na miji ya kisasa, yenye makazi bora na nafuu, miundombinu imara, huduma za kijamii zinazopatikana kwa urahisi pamoja na mazingira salama na rafiki kwa wananchi.

Hayo ni miongoni mwa matarajio yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2050, inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia upangaji na maendeleo endelevu ya miji.

Hayo yamebainishwa Novemba 8, 2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Deogratias Kalimenze wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mipangomiji Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Novemba 8 na mwaka huu siku hiyo inatimiza miaka 77 ya Mipangomiji Duniani.

Amesema, Dira ya Tiafa ya Maendeleo 2050 inaweka msisitizo katika kujenga miji janja (Smart Cities), itakayotumia teknolojia kurahisisha utoaji huduma, kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na kuboresha usimamizi wa rasilimali za mijini.

Kwa mujibu wa Bw. Kalimenze, Tanzania ya 2050 inatarajiwa kuwa na miji yenye makazi bora na yanayomudu gharama za wananchi, maeneo ya kijani yanayolinda mazingira, mifumo bora ya usafiri na usafirishaji pamoja na makazi jumuishi na salama yanayozingatia mahitaji ya makundi yote ya jamii.

Ameeleza kuwa, katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali pia inalenga kujenga miji inayostahimili majanga ya kimazingira, ikiwemo mafuriko na changamoto nyingine zinazoweza kuathiri maisha na shughuli za wananchi.

Akielezea hatua zinazochukuliwa kuelekea mwaka 2050 amesema, Ili kufanikisha maono hayo, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule, masoko, maeneo ya maegesho na majosho.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizaya ya Ardhi, hatua nyingine ni kuweka sera zinazowezesha sekta binafsi kushiriki ujenzi wa nyumba, pamoja na kuimarisha upangaji na upimaji wa ardhi ili kuongeza upatikanaji wa viwanja vilivyopangwa na kupatiwa huduma muhimu.

Vilevile, ameweka wazi kuwa, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanaendelea kuboreshwa katika sekta mbalimbali za Serikali kwa lengo la kurahisisha upatikanaji huduma kwa wananchi na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa miji.

Hata hivyo, Bw. Kalimenze amesema pamoja na jitihada hizo, ukuaji wa makazi yasiyopangwa bado ni changamoto inayokabili miji mingi nchini.

Pia, uhaba wa viwanja vilivyopimwa na kupatiwa huduma muhimu unachangia wananchi kutafuta maeneo ambayo taratibu za upatikanaji wa ardhi ni rahisi zaidi, hata kama hayajapangwa.

Ameitaja sababu nyingine kuwa ni baadhi ya wananchi kuendeleza maeneo bila kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kujenga bila vibali vya uendelezaji ardhi na vibali vya ujenzi.

Bw. Kalimenze amesema, hali hiyo inaonesha kuwa kufikia miji inayotarajiwa mwaka 2050 hakutategemea mipango iliyowekwa pekee, bali pia utekelezaji wake, usimamizi wa matumizi ya ardhi na ushiriki wa wananchi katika kufuata taratibu za mipango miji.

Akizungumzia kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mipangomiji Duniani, amesema kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo yam waka 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Awamu ya Nne wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031 serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuboresha sekta mbalimbali nchini.

Katika maadhimisho hayo, Wataalamu wa Mipangomiji wametakiwa kuendelea kuzingatia misingi ya taaluma yao katika usanifu na uendelezaji wa miji ili kuhakikisha ukuaji wa makazi unazingatia mipango iliyopo na mahitaji ya wananchi.

Kwa ujumla, sura ya Tanzania ya mwaka 2050 itategemea namna maono ya kuwa na miji janja, salama, jumuishi na endelevu yatakavyotekelezwa kuanzia sasa.

Post a Comment

0 Comments