Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha wananchi wanapata makaazi bora, salama na yanayokidhi mahitaji ya maisha ya sasa na yajayo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 08 Novemba 2026, wakati akizindua mauzo ya nyumba za kisasa za Mradi wa Saateni, katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi na kupanua fursa za umiliki wa nyumba.
Ameeleza kuwa sekta ya makaazi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha watumishi wa umma, vijana, wafanyabiashara na wananchi wa kipato cha chini na cha kati kumiliki nyumba kwa masharti nafuu.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi ameelekeza familia zilizopisha maeneo kwa ajili ya mradi huo kuzingatiwa kwa kupatiwa nyumba maalum pamoja na punguzo la asilimia 50 ya kodi, ikiwa ni kutambua mchango wao katika kufanikisha mradi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Sultan Said Suleiman, amesema mradi wa Saateni unatarajiwa kuwa na nyumba 209, maeneo ya biashara, huduma za kijamii na maegesho ya magari. Aidha, familia 25 zilizopisha eneo la mradi zimetengewa nyumba kama sehemu ya kutambua mchango wao.















0 Comments