6/recent/ticker-posts

Kuhakikisha Wananchi Wanapata Huduma Bora za Afya Katika Maeneo Yote ya Zanzibar, Mijini na vijijini.

KAMATI ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi imepokea ripoti ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Afya Zanzibar kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba, ikiwa ni sehemu ya kufuatilia matumizi ya fedha zilizotengwa pamoja na utekelezaji wa mipango na shughuli mbalimbali za Wizara hiyo.

Akizungumza mara baada ya kuwasilisha ripoti hiyo, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, ameeleza matumizi ya fedha zilizotengwa kwa Wizara hiyo katika kipindi husika, sambamba na kueleza hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya sekta ya afya.

Amesema matumizi ya fedha hizo yameelekezwa katika kutekeleza shughuli za Wizara kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika maeneo yote ya Zanzibar, mijini na vijijini.

Aidha, amesema Wizara inaendelea kuzingatia maoni na mapendekezo yanayotolewa na Kamati ya Ustawi wa Jamii, kwa kuyafanyia kazi katika maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya wananchi.

Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Wizara na kamati hiyo ni muhimu katika kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya sekta ya afya, pamoja na kuhakikisha fedha zinazotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi, Hussein Ibrahim Makungu, amesema sekta ya afya ina umuhimu mkubwa katika kuwahudumia wananchi, hivyo kuna haja ya kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji huduma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazokidhi mahitaji yao.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi una nafasi muhimu katika kuimarisha huduma za afya, hususan katika hospitali za wilaya na Mkoa, ambapo ushirikiano huo unaweza kusaidia kuongeza ubora wa huduma na kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuongeza vyuo vikuu vinavyotoa mafunzo ya taaluma mbalimbali za afya ili kuongeza idadi ya wataalamu watakaosaidia kuimarisha huduma katika hospitali na vituo vya afya nchini.

Kwa upande wao, wajumbe wa kamati hiyo wameeleza umuhimu wa kuimarisha utoaji wa elimu hasa katika suala la mikataba   kwa wajumbe pamoja na wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya afya, ili kuongeza uelewa na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika kufuatilia na kuunga mkono juhudi za kuimarisha huduma hizo.

Vilevile, wameeleza umuhimu wa kukamilisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara ya Afya kwa wakati ili iweze kuanza kutoa huduma zilizokusudiwa na kuwawezesha wananchi kunufaika na uwekezaji unaofanywa katika sekta hiyo.

Wamesema kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kupanua wigo wa huduma za afya, kuongeza upatikanaji wa huduma katika maeneo mbalimbali na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi wanapohitaji huduma za matibabu.

mwisho

Post a Comment

0 Comments