6/recent/ticker-posts

SMZ Itaendelea Kuthamini, Kuunga Mkono na Kuhimiza Ushirikiano na Taasisi Mbali Mbali Zinazojitolea Katika Utoaji wa Huduma za Kijamii

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuthamini, kuunga mkono na kuhimiza ushirikiano na taasisi mbali mbali zinazojitolea katika kusaidia utoaji wa huduma za kijamii.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika hafla ya ufungaji wa  kambi ya sita (6) ya matibabu ya Afya bora , Maisha Bora na uzinduzi wa Kampeni ya Oaflad ya "Build Resilience" uliofanyika katika Viwanja vya Kinduni Akademia Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema kambi hio ya matibabu bure ni miongoni mwa juhudi za kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi ambazo zimesogezwa karibu na maeneo yao wanayoishi ili kutoa fursa kwa wananchi kufanya uchunguzi wa afya zao na kupatiwa matibabu bila ya malipo yoyote.

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa katika kambi ya sita ya matibabu ya Afya bora maisha bora huduma mbalimbali za matibabu na uchunguzi wa afya zimetolewa ikiwemo upasuaji mdogo, afya ya uzazi, saratani, magonjwa ya moyo, uchunguzi wa magonjwa ya ngozi, matibabu ya macho pamoja na magonjwa yakuambukiza na yasiyo yakuambukiza.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewahimiza wananchi kuendelea kufanya mazoezi ili kuboresha afya ya mwili na akili, kujenga tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara pamoja na kufuata maeleekezo ya wataalamu wa Afya ambayo yatawasaidia kubaini tatizo katika hatua za awali ambazo ni rahisi kupatiwa matibabu.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameipongeza Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation chini ya uongozi wa Msarifu na Mwenyekiti wake Mama Mariam Mwinyi kwa kuendelea kujitolea kutoa huduma za afya bila ya malipo katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar ikiwa ni jitihada za kuunga mkono serikali kupitia Sekta ya Afya ambayo inamgusa kila mwananchi wa Zanzibar.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza wafadhili na wahisani waliofanikisha kufanyika kwa kambi ya sita ya matibabu ya Afya bora Maisha bora pamoja na kuwapongeza madaktari wazawa na wageni ambao  wamejitolea kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa kaskazini Unguja wananufaika na matibabu yanayotolewa kambini hapo.

Nae Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amewataka wananchi waliobainika na changamoto za kiafya kufika katika vituo vya Afya na Hospitali mbali mbali kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi ili kujiepusha na athari kubwa zinazoweza kujitokeza kwa kushindwa kupatiwa matibabu mapema.

Amesema muitikio wa wananchi katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation umekuwa mkubwa hasa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ambako idadi ya wananchi waliofika kambini hapo kuchunguza afya zao na kupatiwa matibabu inaongezeka maradufu na kuiwezesha kambi hio kitimiza malengo yake ya kuwafikia zaidi ya wananchi Elfu Tano ( 5000 ).

Akisoma taarifa ya Kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji amesema lengo la Kufanyika kwa kambi ya Matibabu ya Afya bora Maisha bora ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, kupata fursa ya kuchunguza afya zao na kupatiwa matibabu hapo hapo endapo mwananchi atagundulika na tatizo lolote.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuekeza katika miundombinu ya Afya pamoja na kuimarisha matibabu bingwa na bingwa bobezi ili kuweza kutoa huduma bora za afya na kuhakikisha ustawi bora wa wananchi unazidi kuimarika siku hadi siku.

Dkt. Mngereza amefahamisha kuwa azma ya Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030  huduma zote za uchunguzi wa magonjwa mbali mbali na matibabu ya kibingwa yanapatikana Zanzibar ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kufuata huduma hizo nje ya Zanzibar lakini pia kuwapunguzia gharama za kulipia matibabj hayo.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation Bi. Rehema Tukai amesema kambi ya sita ya matibabu ya Afya bora maisha bora itakuwa endelevu katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar ambapo Taasisi hio imejipanga kuwapatia huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi zaidi ya elf Tano ( 5000 ) waliofika kambini hapo kwa ajili ya kuchunguza afya zao.

Tukai emesema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya  kambi hio imeweza kutoa huduma za uchunguzi wa matibabu ya magonjwa ya moyo, saratani, upasuaji mdogo, Afya ya uzazi, macho, ngozi pamoja na magonjwa yakuambukiza na yasiyo yakuambukiza.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR )

Leo....tarehe 07. 11. 2026

Post a Comment

0 Comments