6/recent/ticker-posts

SMZ Itaendelea Kuwekeza Katika Ujenzi na Uimarishaji wa Miundombinu ya Sekta ya Afya Ili Kuimarisha Huduma za Afya Zenye Ubora

WAZIRI wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwekeza katika ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya sekta ya afya ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya zenye ubora kwa wananchi.

Amesema hayo wakati wa ziara maalumu ya kutembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya afya, ikiwemo mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja na mradi wa Mwembeladu, na vituo vya afya ambapo ameridhishwa na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kuimarisha miundombinu itakayowezesha wananchi kupata huduma kwa wakati, kuongeza ufanisi katika utoaji wa matibabu na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi wanapohitaji huduma za afya.

Akizungumzia maendeleo ya mradi wa Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja, Waziri Mazrui amesema matarajio ya Serikali ni kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ifikapo Novemba 2027, ili miundombinu hiyo iweze kuanza kutumika na kuongeza uwezo wa hospitali hiyo katika kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi.

Ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na washirika wa maendeleo, wakiwemo Saudi Fund, Kuwait Fund na BADEA, ambao wamechangia katika juhudi za kuimarisha miundombinu ya huduma za afya Zanzibar.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha huduma zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja, hivyo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya zilizo bora na zinazokidhi mahitaji yao.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Mbarouk Hamad Mbarouk, amesema utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri na kwamba hadi sasa umefikia asilimia 29.8 ya hatua za ujenzi.

Amesema timu inayosimamia mradi huo inaendelea na kazi kwa lengo la kuhakikisha shughuli za ujenzi zinakamilika kwa kuzingatia muda uliopangwa, huku matarajio yakiwa ni kukamilisha mradi huo mwishoni mwa mwaka 2027.

Ameeleza kuwa ushirikiano unaoendelea kati ya Serikali na washirika wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa na kukamilika kwa wakati, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Mradi wa Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja na vituo vya afya ni miongoni mwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya na kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma kwa wananchi, sambamba na kuboresha ubora wa huduma za matibabu nchini.

Post a Comment

0 Comments