6/recent/ticker-posts

WAZIRI DKT. RIZIKI PEMBE AITAKA ZICOO KUWA CHACHU YA MABADILIKO KATIKA TAASISI ZA SERIKALI

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma, akizungumza na Viongozi wa Jumuiya ya Maafisa habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICOO) wakati Uongozi wa Jumuiya hiyo ulipofika Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini kwa ajili ya kujitambulisha na kuelezea mikakati mbalimbali ya utendaji wa Kazi zao.

Wilaya ya Mjini, Zanzibar. 20 /10/2026.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma, ameitaka Jumuiya ya Maafisa Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICOO) kuleta mabadiliko kwa kufanya kazi kwa vitendo na ubunifu ili kuimarisha taswira ya taasisi zao pamoja na Serikali kwa ujumla.

Ameyasema hayo baada ya kupokea ugeni wa viongozi wa Jumuiya hiyo uliofika ofisini kwake Migombani, Wilaya ya Mjini, kwa lengo la kujitambulisha na kueleza shughuli zinazotekelezwa na jumuiya hiyo.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, hivyo ni muhimu kwa ZICOO kuwa mstari wa mbele katika kuitangaza miradi hiyo ili wananchi waweze kupata taarifa sahihi na kuelewa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuwaletea maendeleo.

Aidha, ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, itaendelea kushirikiana na jumuiya hiyo ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo iliyojiwekea.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maafisa Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICOO), Raya Hamad Suleiman, amesema lengo la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuwaunganisha maafisa habari na mawasiliano ili waweze kufanya kazi kwa ushirikiano na kuwa na sauti moja katika kutekeleza majukumu yao.

Amesema kuwa miongoni mwa malengo mengine ya jumuiya hiyo ni kubaini fursa mbalimbali zilizopo, ikiwemo za mafunzo, pamoja na kutambua changamoto zinazowakabili wanachama wake na kuziwasilisha katika mamlaka husika kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Ameongeza kuwa jumuiya hiyo inalenga kuimarisha mawasiliano na ushirikiano miongoni mwa maafisa habari ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa taarifa kwa umma na kuimarisha taswira ya taasisi wanazozihudumia.

Akitoa shukrani katika ziara hiyo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maafisa Habari Zanzibar, Makame Khamis Mohammed (Utani), ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kufikia malengo yaliyopangwa katika kusaidia Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Aidha, amesema maafisa habari katika Taasisi za Serikali za Mapinduzi ya Zanzibar wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuleta tija katika taasisi zao.

Ameeleza kuwa maafisa hao wanapaswa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa vitendo na kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu shughuli na mafanikio ya taasisi zao, hatua itakayosaidia kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi.

Jumuiya ya Maafisa Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICOO) ilianzishwa mwaka 2024 ukiwa na wanachama  zaidi ya 100.

Imetolewa na Kitengo cha Habari,
WHSUM.

Post a Comment

0 Comments