6/recent/ticker-posts

Ufadhili wa Benki ya Dunia Katika Awamu ya Kwanza Umekuwa na Mchango Mkubwa Katika Kuimarisha Huduma za Afya Zanzibar


WIZARA ya Afya Zanzibar na Benki ya Dunia zimejadili maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya afya iliyofadhiliwa katika awamu ya kwanza, pamoja na uwezekano wa kupata ufadhili wa ziada wa dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kipaumbele, ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto katika eneo la Kilimani na kuimarisha huduma za Damu Salama.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, wakati alipokutana na  ujumbe wa Benki ya Dunia uliofika ofisini kwake kwa lengo la kutathmini maendeleo ya miradi iliyotekelezwa, kujadili mafanikio yaliyopatikana na kuweka mikakati ya kuendeleza ushirikiano katika awamu inayofuata.

Akizungumza katika mazungumzo hayo, Waziri Mazrui amesema ufadhili wa Benki ya Dunia katika awamu ya kwanza umekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha huduma za afya Zanzibar, ikiwemo upatikanaji wa magari ya kubebea wagonjwa, vifaa vya Bohari Kuu ya Dawa, dawa na ujenzi wa vituo vya afya.

Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo ya Fuoni na Jang’ombe, pamoja na kuendelezwa kwa ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya katika Kivunge na Micheweni, Pemba, hatua zinazolenga kuimarisha mazingira ya kazi kwa wataalamu wa afya na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Amefahamisha kuwa ujumbe huo ni muhimu katika kufuatilia utekelezaji wa miradi, kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unaleta matokeo yaliyokusudiwa katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kupata ufadhili wa ziada wa dola za Marekani milioni 100 katika awamu inayofuata kwa ajili ya kuendeleza miradi ya kipaumbele, ambayo itasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo na kuongeza uwezo wa sekta ya afya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesema miongoni mwa miradi inayolengwa ni ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto katika eneo la Kilimani, Zanzibar, ambayo inatarajiwa kuongeza uwezo wa Serikali kutoa huduma za afya ya uzazi na watoto, ikiwemo huduma kwa wajawazito, wanawake wakati wa kujifungua na watoto wanaohitaji uangalizi na matibabu maalumu.

Amefafanua kuwa kuimarishwa kwa huduma hizo kutasaidia kuimarisha huduma za mama na mtoto na kuchangia juhudi za Serikali za kupunguza vifo vya mama wajawazito, watoto wachanga na watoto vinavyoweza kuzuilika kupitia huduma bora na kwa wakati.

Aidha, amesema mipango ya awamu inayofuata inajumuisha kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya kupitia mafunzo kwa wahudumu mbalimbali, wakiwemo wakunga na wauguzi, ili kuongeza ujuzi wao wa kitaaluma na kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya afya.

Kwa upande  huduma za damu salama, Waziri Mazrui amesema Serikali inalenga kuimarisha huduma za Damu Salama kwa kuhakikisha kunapatikana vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya ukusanyaji, uchunguzi, uhifadhi na usambazaji wa damu kwa wagonjwa wanaoihitaji.

Amefahamisha  kuwa uwekezaji katika miundombinu ya afya, upatikanaji wa vifaa tiba na mafunzo kwa wataalamu ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha mfumo wa afya na kuongeza uwezo wa vituo vya kutolea huduma kukidhi mahitaji ya wananchi, sambamba na kuendeleza Zanzibar kuwa kitovu cha huduma bora za afya na utalii wa tiba.

Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya Dunia anayesimamia masuala ya Sera za Afya katika Kanda ya Afrika Mashariki, Ernest Massiah, amesema wamefurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza miradi inayolenga kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Amesema Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya, kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo na vipaumbele vilivyowekwa ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na manufaa kwa wananchi.

Ameeleza kuwa tathmini ya miradi iliyotekelezwa katika awamu ya kwanza itasaidia kubaini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele katika mipango ya baadaye, ili kuimarisha ufanisi wa uwekezaji katika sekta ya afya.

Ushirikiano huo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Dunia unalenga kuendeleza juhudi za kuboresha miundombinu ya afya, kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu na kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zinazokidhi mahitaji yao.

Mwisho.

 

Post a Comment

0 Comments