Na Vicent Marwa,Simiyu
Mbunge wa jimbo la Kisesa (CCM) wilayani Meatu,
mkoani Simiyu, Luhaga Mpina na Mkuu wa wilaya hiyo, Rosemary Kirigini, wametoa
pikipiki 25 zenye thamani ya shilingi milioni 55 kwa Chama Cha Mapinduzi
wilayani humo.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Mpina
alisema pikipiki hizo zitagawiwa kwa Makatibu wa kata wa CCM katika wilaya hiyo
kwa lengo la kuimarisha shughuli za chama.
“Sisi tukiwa makada wa CCM kwa pamoja tumeamua
kushirikiana kwa pamoja na tukapata pikipiki hizi 25 kwa kila Kata zilizoko
ndani ya wilaya yetu hivyo tumeona tuwapatie Makatibu wa Kata ili tuboreshe
utendaji kazi wao,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya hiyo,Kirigini
ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum CCM mkoa wa Mara, alisema ni vizuri
pikipiki hizo zikatumiwa kama zilivyokusudiwa
na siyo kuzigeuza boda boda.
Akishukuru kwa niaba ya Makatibu kata,Katibu wa
CCM kata ya Mwanhuzi, Mawazo Shabani, alisema mbali na kuwapongeza viongozi hao
aliongeza kuwa sasa utendaji wa kazi zao utakuwa rahisi kwani wataweza kufika
maeneo yao kwa
wakati.
Diwani wa kata ya Mwanhuzi, Eliya Shukia akizungumza
kwa niaba ya CCM wilayani humo pia aliwashukuru viongozi hao kwa kitendo
walichokifanya na kueleza kuwa huo ni
mwanzo mzuri wa chama hicho kuelekea katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa
na uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwakani.
0 Comments