6/recent/ticker-posts

Mabadiliko Makubwa ya Sayansi na Teknolojia ni Lazima Kuekeza Katika Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Amali

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi Johnson Andrew Tumaini zawadi ya mfanano wa Hundi ya shilingi laki tano (500,000) akiwa muhitimu bora Katika fani ya Ufundi Stadi wa Madawa katika Mahafali ya Pili ya Chuo cha Glorious Polytechnic College yaliyofanyika katika Viwanja vya Mao Zedong Kikwajuni Zanzibar.

Taasisi za elimu nchini zimetakiwa kuekeza katika kutoa elimu inayounganisha nadharia na vitendo ili wahitimu wawe na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangia kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika Mahafali ya Pili ya Chuo cha Glorious Polytechnic College Zanzibar,yaliyofanyika katika Viwanja vya Mao Zedong Kikwajuni Wilaya ya Mjini Unguja.

Amesema ili kuendana na mabadiliko makubwa ya Sayansi na Teknolojia ni lazima kuekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo ya amali ambayo ina nafasi kubwa katika kuwaandaa vijana kukidhi mahitaji ya soko la ajira, kujiajiri na kuwawezesha kutumia maarifa yao katika kuleta maendeleo katika jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wahitimu hao kuangalia fursa zilizopo katika Sekta za Umma na Binafsi  pamoja na kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kubuni fursa mbali mbali zitakazowawezesha kujiajiri wenyewe na kuepuka mtazamo hasi wa kwamba mafanikio yanatokana na kuajiriwa Serikalini ama katika sekta Binafsi.

Sambamba na hayo amewasisistiza wahitumu suala zima la nidhamu, uwajibikaji, uaminifu, unyenyekevu na  kujijenga katika tabia njema kwa kutanguliza utu wakati wa utoaji wa huduma kwa jamii unazozingatia sheria, kanuni, miiko na taratibu za utumishi. 

Mhe. Hemed amewasihi wahitimu wanaomaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali  kuendelea kujifunza na kujiendeleza katika ngazi za elimu ya juu sambamba na  kuitumia taaluma waliyoipata kwa  kufanya kazi kwa vitendo ili kuweza kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu hasa wanaohitimu masomo yao kujenga utayari wa kurejesha mikopo waliyopatiwa ili kutoa fursa kwa wananfunzi wengine kupatiwa mikopo hio itakayowawezesha kusoma kwa utulivu.

Lela amefahamisha kuwa Wizara ya elimu Zanzibar kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kuanzia ngazi ya astashahada hadi ngazi ya uzamili kwa lengo la kuwawezesha kusoma katika mazingira rafiki yatakayochangia kuongezeka kwa wataalamu wa fani mbalimbali  watakaolitumikia Taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Glorious Polytechnic College Dkt.Idrisa Muslih Hija amesema chuo hicho kimekuwa kikoshirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Elimu na Taasisi nyengine za elimu ili kuhakikisha taaluma inayotolewa chuoni hapo inaendana na mabadiliko makubwa ya Sayansi na Teknolojia, uhitaji wa soko la ajira na ushindani wa kibiashara katika sekta ya elimu ya juu na vyuo vya kati.

Dkt. Muslih amesema chuo cha Glorious Polytechnic kimedhamiria kuendelea kutoa elimu inayozingatia viwango na ubora katika fani zinazofundishwa chuoni hapo ili kuwajengea uwezo wahitimu kuweza kujifunza kutokana na uhalisia wa mazingira ya kazi sambamba na kuwajengea uwezo wa kuweza kujitegemea.

Aidha, Dkt Muslih ameahidi kuwa Chuo hicho kitaendelea kushirikiana na Wizara ya elimu na wadau wote wa sekta ya elimu katika kuhakikisha sekta ya elimu nchini inazidi kukua na kuimarikana ili lengo la kuwa na wataalamu wabobezi katika fani mbalimbali mbali linafikiwa.

Mapema akisoma Risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, muhitimu Omar Said Suleiman ameahidi watakuwa wazalendo wa kweli, waammifu na kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia  elimu, maarifa na ujuzi walioupata kwa manufaa ya jamii, Zanzibar na Taifa kwa ujumla.

Wahitimu hao wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kuimarisha program za mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu, kuwezesha upatikanaji wa mikopo nafuu na ruzuku kwa vijana wabunifu pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo, Sekta binafsi na Taasisi za Umma jambo litakalosaidia kukuza  Sekta ya elimu nchini.

Katika Mahafali hayo jumla ya wannafunzi 478 wamehitimu masomo yao katika fani mbali mbali ikiwemo fani ya Afisa Tabibu, Fundi Stadi wa Madawa, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ngazi ya tatu, Usaidizo wa Maabara ya Viwanda Ngazi ya Tatu, Usaidizi wa Uendeshaji wa Biashara na Wasaidizi wa Maabara.

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe  08 / 11 / 2026

Post a Comment

0 Comments