6/recent/ticker-posts

Timu ya 36 ya Madaktari Kutoka Nchini China Wawasili Zanzibar kwa Ajili ya Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Matibabu Katika Hospitali za Unguja na Pemba

Na.Mwandishi Wizara ya Afya Zanzibar.

WIZARA ya Afya Zanzibar imepokea timu ya 36 ya madaktari kutoka nchini China waliofika Zanzibar kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali za Unguja na Pemba, hatua inayolenga kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza na madaktari hao waliofika Wizara ya Afya kwa ajili ya kujitambulisha, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema Zanzibar na China zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika sekta ya afya, unaoendelea kuimarisha ushirikiano na kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.

Amesema ushirikiano huo ni sehemu muhimu ya juhudi za kuendeleza sekta ya afya Zanzibar, akieleza kuwa wananchi wana imani kubwa na mchango wa madaktari hao katika kuwahudumia wagonjwa na kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa afya nchini.

Waziri Mazrui amefahamisha kuwa madaktari hao watashiriki katika kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wenye maradhi mbalimbali, sambamba na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa afya wa Zanzibar kupitia mafunzo na ushirikiano wa kitaalamu.

Ameeleza kuwa uwepo wa madaktari hao katika hospitali za Unguja na Pemba utasaidia kuimarisha huduma katika maeneo mbalimbali ya matibabu, pamoja na maeneo mengine kulingana na utaalamu wao.

Kwa upande wake, kiongozi wa timu hiyo ya madaktari kutoka China Wang Wei amesema wataendelea kushirikiana na wataalamu wa afya wa Zanzibar katika kutoa huduma kwa wananchi, akisisitiza dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya pande hizo mbili.

Amesema timu hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na watumishi wa sekta ya afya ili kusaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi wa Unguja na Pemba.

Ushirikiano huo kati ya Zanzibar na China unaendelea kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya afya, kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kitaalamu, pamoja na kuongeza fursa za wananchi kupata huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali hapa nchini.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments