Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejiandaa vyema kuwapokea kwa heshima vijana wa timu ya Zanzibar Spice Boys walioibuka mabingwa katika mashindano ya kimataifa ya soka kwa watoto ya PQCUPBRASIL 2026 yaliyofanyika nchini Brazil.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hafla fupi ya kutangaza ratiba ya mapokezi ya vijana hao, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Migombani, Zanzibar.
Amesema vijana hao watapokelewa rasmi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar, saa nane mchana, baada ya kurejea kutoka nchini Brazil.
Dkt. Riziki amewahimiza wananchi, viongozi, wadau wa michezo na vijana wa rika mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi hayo ili kuwapongeza vijana hao kwa mafanikio makubwa waliyoyapata na juhudi zao za kuipeperusha vyema bendera ya Zanzibar na Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Amesema mapokezi hayo ni ishara ya kuthamini vipaji vya vijana na kutambua mchango wa michezo katika kuitangaza nchi kimataifa, huku yakitarajiwa kuwa chachu ya kuwahamasisha vijana wengine kujituma na kutumia vipaji vyao kujiletea maendeleo.
Ameeleza kuwa kikosi cha Zanzibar Spice Boys kilijumuisha wachezaji chipukizi 18 wenye umri wa miaka 12 na 13, walioshiriki mashindano ya PQCUPBRASIL 2026 yaliyofanyika nchini Brazil kuanzia Oktoba 10 hadi 15, 2026.
Amesema mashindano hayo yalishirikisha timu mbalimbali kutoka Brazil, Ureno, Argentina na mataifa mengine, hali iliyowapa vijana hao fursa ya kupima uwezo wao, kujifunza mbinu mpya za mchezo wa soka na kupata uzoefu wa kushindana katika medani ya kimataifa.
Amebainisha kuwa wachezaji hao wameonesha uwezo wao mkubwa wa vipaji vyao katika ushindani wa hali ya juu uwanjani, sambamba na kufunga mabao mengi katika mashindano hayo, jambo linalodhihirisha juhudi na maandalizi waliyoyafanya kabla ya kushiriki mashindano hayo.
Aidha, amesema mapokezi ya vijana hao yataambatana na burudani kutoka katika vikundi mbalimbali, vitakavyoshiriki kuwashangilia kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Kwa Machina hadi Kisonge, ikiwa ni sehemu ya kuwapongeza kwa mafanikio yao.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono maendeleo ya vijana kupitia michezo na kuhakikisha kuwa wanapata fursa ya kuendeleza vipaji vyao sambamba na masomo, ili kuwajengea msingi imara wa maisha yao ya baadaye.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (WHSUM)
.jpeg)
.jpeg)
0 Comments