6/recent/ticker-posts

TCRA yajipanga kuliwezesha Jeshi la Polisi kukabiliana na matumizi ya mabaya mtandao

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wake Dr. Ally Yahya Simba wa Pili kutoka Kushoto.

Wa kwanza kushoto ni Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Kanda ya Zanzibar Bwana Othman Sharif.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania            { TCRA } Dr. Ally Yahya Simba wa Pili kutoka Kushoto akifafanua jambo wakati timu yake ilipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } imejipanga kuliwezesha  Kitaaluma Jeshi la Polisi Nchini katika azma yake ya kukabiliana na wimbi jipya la matumizi mabaya ya mitandao ya mawasiliano linaloonekana kushika kasi katika maeneo mbali mbali Duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania  Dr. Ally Yahya Simba alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Mtaa wa  Vuga Mjini Zanzibar.

Dr. Ally Yahya Simba akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Watatu wa Taasisi  hiyo na kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo Tarehe 6 Julai mwaka huu alisema Mamlaka ya Mawasiliano  kwa mujibu wa sheria ina jukumu la kufuatilia makosa ambayo tayari yameshafanywa kwenye Mitandao.

Alisema Jeshi la Polisi ndilo lenye haki ya kufungua kesi kwa wahusika wa makosa ya Mitandao  jambo ambalo askari wa Jeshi hilo wanapaswa kuwa na elimu ya kutosha  itakayowapa uwezo mkubwa wa kukabiliana na wahusika wa makosa hayo.

Alifahamisha kwamba  zipo  Kesi Nne zinazohusu matumizi mabaya ya Mitandao hiyo ambazo zinatarajiwa kutolewa maamuzi yake hivi karibuni na vyombo vinavyohusika kufuatia kupitishwa kwa  sheria ya matumizi ya mitandao ya Mawasiliano Nchini  kulikofanywa na Bunge ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } Dr. Ally Yahya Simba aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa  uamuzi wake wa kuipatia Mamlaka hiyo eneo la Kiwanja kwa ajili ya kujenga Ofisi yake hapa Zanzibar.

Dr. Ali alisema hatua hiyo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeipa  nguvu Mamlaka hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi  zaidi katika Visiwa vya  Zanzibar  vikiwa ni miongoni mwa Kanda Tano zinazojumuisha na kuunda Mamlaka hiyo Nchini Tanzania.

Mapema Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania  { TCRA }Kanda ya Zanzibar Bwana  Othman Sharif alisema yapo mafanikio makubwa  ya zaidi ya asilimia 99% tokea kuanzishwa kwa mradi mpya wa Mawasiliano { post cort } katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Bwana Othman alisema mradi huo umetekelezwa katika shehia Nne  Hapa Zanzibar akizitaja kuwa ni Selemu na Dimbani kwa Kisiwa cha Pemba pamoja na  Mombasa na Chukwani kwa Kisiwa cha Unguja.

Meneja huyo wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Kanda ya Zanzibar  aliishukuru Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano  Zanzibar pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa mashirikiano makubwa  ilizotoa katika kufanikisha mradi huo muhimu kwa ustawi wa Jamii Nchini.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inaendelea kuzihimiza Taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kufungua Ofisi zao Zanzibar.

Balozi Seif alisema hatua hiyo ya ufunguzi wa Ofisi pamoja na huduma za Taasisi hizo italenga  katika ile azma ya  Waasisi wa Taifa hili ya  kutaka kuimarisha Muungano wa Mwezi Aprili mwaka 1964 uliofanywa na pande hizo mbili za Muungano wa Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { TCRA } kwa jitihada zake za kuanzisha mradi mpya wa mawasiliano    { Post cort }utakaosaidia kwa kiasi kikubwa ulinzi wa Maeneo pamoja na mazingira.

Hata hivyo Balozi Seif alifahamisha kwamba zipo changamoto za baadhi ya Mitaa  pamoja na Majina yake kujengwa  au kuanzishwa bila ya utaratibu wa kuzingatia Mipango miji pamoja na Halmashauri za Wilaya.

Post a Comment

0 Comments