Na Haji Nassor, Pemba
Baada ya kampuni ya MECCO kusimamisha ujenzi wa
barabara za Gando na Konde kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, sasa ujenzi huo
umenza tena, kwa matengenezo ya sehemu zilioathirika, baada ya kukabidhiwa
zaidi ya shilingi bilioni tano.
Awali ujenzi wa barabara hizo, ulianza tokea mwaka
2009 na kampuni hiyo kusitisha ujenzi wake kutokana na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na washirika wake Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Mfuko wa Saudi
Arabia, kutoingiza fedha kwa wakati.
Uchunguzi umebaini mara baada ya kusaiini mkataba
wa ujenzi wa barabara hizo, kampuni ya MECCO ilianza ujenzi Septemba 1, 2009 na
ilitakiwa kukamilisha ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami, Januari 1,
2012.
Hata hivyo, kazi hiyo ilishindikana kutokana na
kujitokeza mambo kadhaa na baadae kampuni hiyo iliomba kuongezewa miezi nane
zaidi, ambapo iliahidi kumaliza ujenzi huo Agosti 27, 2012 ingawa pia haikumaliza.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia
simu, Ofisa Mdhamini wa wizara hiyo, Hamad Ahmed Baucha, alikiri kwamba kwa
sasa ujenzi huo umeanza na utaendelea moja kwa moja hadi kukamilika kwa kiwango
cha lami.
Alisema ujenzi wa barabara ya Wete- Gando na
Wete-Konde umeanza hasa katika maeneo yaliyoharibika kutokana na kukatika kwa
mvua.
Alisema hivi karibuni MECCO, ilishakabidhiwa
shilingi bilioni tatu kwa mara ya kwanza na mara ya pili hakumbuki ni kiasi
gani ilipewa lakini jumla ni zaidi ya shilingi bilioni tano.
Mhandishi kutoka wizara ya Miundombinu na
Mawasiliano anaefuatilia ujenzi huyo, Rashid Issa Rashid, alisema kwa sasa
ujenzi huo umeanza taratibu na ana matumanini kwamba, utaendelea hadi kumalizia
kwa kiwango cha lami.
“Nilisikia kwamba MECCO wameshatimiziwa madai yao
ya fedha, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi na waondoe hofu, kwani wizara kwa
kushirikiana na washirika wake wa maendeleo, inayo nia thabiti ya kuwatandikia
wananchi lami,’’alisema.
Katika hatua nyengine, Ofisa Mdhamini huyo alisema
hakuna hata nyumba moja iliovunjwa wakati huo wa ujenzi na ambayo mmiliki wake
hajalipwa fidia.
Alibainisha kuwa kilichobakia ambacho hakijalipwa
ni zile nyumba zilizoharibika wakati wa ujenzi pamoja na fidia kwa miti iliyokatwa
na vipando vilivyoharibika.
Aliwataka wananchi wa maeneo mbalimbali kuendelea
kuwa wastahamilivu na serikali kamwe haijasahau kuwapa haki zao.
Baadhi ya wananchi wanaotumia barabara hizo walisema
pamoja kwamba kampuni imeanza kazi, bado hawana hakika kwamba barabara zao
zitamalizika kwa kiwango cha lami kutoka na kampuni hiyo kufanya kazi kwa kusua
sua.
Kampuni ya ujezi wa barabara ya MECCO ilianza
ujenzi wa barabara za Wete–Gando na Wete–Konde zenye urefu wa kilomita 30,
mwaka 2009 na ikitarajiwa kukabidhi kwa serikali Januari 1, mwaka 2012.
0 Comments