Na Judith Mpalanzi, Kilombero
Kivuko cha mto Kilombero kinachotumika kuvusha
watu na mizigo kutoka na kwenda Ulanga, kimesombwa na maji na kumlazimu Mwenyekiti
wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Kilombero na Ulanga, Francis Mitti,
kupiga marufuku shughuli za kusafirisha abiria.
Marufuku hiyo inatokana na mto huo kuongezeka maji
na kina hivyo kuhatarisha usalama wa vyombo vinavyovusha watu na malizao.
Uamuzi wa kusitishwa huduma hiyo, inatokana na Kaimu
Mkuu wa kivuko cha mto Kilombero, Mhandisi Faustin Magembe, kumwomba Mwenyekiti
huyo kukifunga kwa usalama wa watu na mali zao.
Akitangaza kufungwa kwa kivuko hicho, Mwenyekiti
huyo ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, alisema wananchi wa pande hizo
watalazimika aidha kuzungukia mkoani Iringa au kubaki walipo hadi maji
yatakapopungua.
Aidha alipiga marufuku matumizi ya kuvua au kuvuka
kwa mitumbwi na kuagiza halmshauri ya Kilombero na Ulanga kutenga fedha za
kutosha kununua boti zitakazotumika kuvushia abiria hususani kipindi hiki cha
masika.
Akionesha kusikitishwa na kusombwa kwa kivuko
hicho, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wanachi kuachana na uvuvi kipindi hiki
hadi hapo hali itakapobadilika.
Kwa upande wake, Meneja wa Tanroads mkoa wa
Morogoro, Doroth Mtenga, alisema kukatika kwa barabara baada ya kalavati
kusombwa na maji shughuli yake itachukua muda kidogo kwani haiwezekani kwa hali
iliyopo kurudishia karavati eneo hilo
tokana na kasi ya maji iliyopo.
0 Comments