6/recent/ticker-posts

Waamuzi wala rushwa kikaangoni

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
 
CHAMA cha Waamuzi wa Soka Tanzania Bara (FRAT), kimesema kinafanyia kazi tuhuma za waamuzi wake kupokea rushwa kwa ajili ya kuzibeba baadhi ya timu zinazowahonga katika ligi kuu inayoendelea.
 
Mwenyekiti wa FRAT Joan Minja, amesema mjini Dar es Salaam jana kuwa, chama chake kimekuwa kikipokea tuhuma hizo mara kwa mara kutoka kwa wadau wa soka hivyo kimeona ni vyema wazifanyie kazi ili kubaini ukweli.
 
Joan alisema tuhuma zozote zinazohusiana na rushwa ni nzito na zinapaswa kuchunguzwa kwanza ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa uthibitisho kabla ya kutolewa uamuzi.

Alisema baada ya kuzifanyia kazi tuhuma hizo, FRAT inatarajia kuwasilisha ripoti kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya maamuzi zaidi. "Hatuwezi kutoa ripoti za uchunguzi wetu kwa vyombo vya habari, tutafanya hivyo kwa TFF kwa sababu ndicho chombo tunachofanya nacho kazi", alisema Minja.
 
Timu kadhaa zinazoshiriki katika michuano ya ligi kuu, zimekuwa zikiwalalamikia baadhi ya waamuzi kwa madai kuwa, wamekuwa wakichezesha kwa upendeleo kutokana na kupewa rushwa.
 
Tayari kamati ya ligi imeshatangaza kuwasimamisha baadhi ya waamuzi na kuwaondoa kwenye ligi kwa madai ya kuvurunda katika baadhi ya mechi.
 
Mmoja wa waamuzi waliofungiwa ni Mathew Akrama kutoka Mwanza, aliyechezesha mechi ya ligi hiyo kati ya Simba na Yanga, Oktoba 3 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Post a Comment

0 Comments