6/recent/ticker-posts

DK BILAL ATEMBELEA MAENEO YA MABOMU

Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal ametembelea kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) namba 511 cha Gongo la Mboto ambako kumetokea milipuko mikubwa ya mabomu.

Akiwa katika eneo la tukio alipata maelezo ya namna mabomu hayo yalivyoripuka na hasara iliyopatikana ikiwa ni pamoja na vifo vya watu zaidi ya 20 kutokana na majeraha ya mabomu na wengine msituko.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa kikosi hicho Kanali Aloyce Mwanjile alimweleza Makamu wa Rais kuwa jitihada zinafanywa na wataalamu wa jeshi hilo kwenda kwenye maeneo mbali mbali ambayo mabomu hayo yanadaiwa kutapakaa ili kuyaondoa.

Kanali Mwanjile ameyataja maeneo hayo ambayo mengi ni yale yaliyo jirani na kambi hiyo kuwa ni pamoja na uwanja wa ndege, Gongo la Mboto, Majohe,Pugu Kajiungeni, Kinyerezi na kuna taarifa kuwa mabomu hayo yamefika hadi Kwembe.

Ameeleza pia kuwa jitihada zinafanywa na jeshi hilo kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa jeshi mara waonapo mabomu hayo au vitu ambavyo wanavitilia mashaka na kubainisha pia kuwa nje ya kambi hiyo wameweka kituo maalum cha wananchi kutolea taarifa kama hizo.

Katika ziara hiyo alikuwepo pia Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali Abdulrahaman Shimbo.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais

Dar es salaam

Alhamisi – Februari 17, 2011

Post a Comment

0 Comments