6/recent/ticker-posts

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla Amefungua Masjid Qubah Kwa Niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akikata Utepe kwa Niaba ya Hajjat Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kuashiria ufunguzi wa Masjid QUBA uliopo Kisiwani Kwa Binti Abedi Wilaya ya Wete , Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hajjat. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Misikiti ni sehemu muhimu ya kuunganisha Waumini Katika kutekeleza Ibada mbali mbali kama lilivyo lengo la kuumbwa kwao.

Hajjat Dkt. Samia ameyasema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa Niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla katika Ufunguzi wa Masjid Quba na Madrasa kisiwani kwa Bint Abed Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema kuwa Misikiti ina nafasi kubwa katika kuijenga Jamii kuwa na Maadili mema ambapo amewataka Waumini wa Mskiti huo kuanzisha Darsa kwa Rika zote, kuimarisha umoja, upendo na mshikamano ili kupata Jamii yenye hofu juu ya Allah.

Hajjat. Dkt. Samia amewasihi viongozi wa Mskiti huo kuhakikisha wanautunza kwa kuufanyia usafi nje na ndani ili uendelee kuwa na haiba yake na kuweza kutumika kwa muda mrefu na kuleta faida vizazi hadi vizazi.

Rais Samia ameishukuru Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuzitambua na kuzisimamia Madrasa na Misikiti ili Waislamu waweze kufanya Ibada kwa utulivu pasipo na mivutano ya aina yoyote.

Sambamba na hayo ametumia fursa hiyo kuwaasa Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya Mvua za vuli zinazotabiriwa kuambatana na Elnino na kueleza kuwa ni vyema kufuata maelekezo ya Mamlaka ya hali ya hewa ya hewa Tanzania (TMA) ikiwemo kuhama katika maeneo hatarishi.

Aidha, amewataka Wananchi Kuendelea kulinda, kudumisha na kuimarisha Amani na utulivu ili kuipa  nafasi Serikali kuendelea kutimiza malengo yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Alhajj Shekh Mahmoud Mussa Wadi ameeleza kuwa ujenzi wa Misikiti ni katika dalili za kumcha Mungu ambapo kuna ujira Mkubwa ndani yake ikiwemo makazi mema mara baada ya maisha ya duniani.

Ameeleza kuwa ni jukumu la Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ni kusimamia Mskiti huo ili uendelee kutunzwa na kudumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya vizazi hadi Vizazi.

Akisoma Taarifa ya ujenzi huo Ndugu Yussuf Kaisa Makame kutoka kampuni ya Skyline Construction Co. Ltd ameeleza kuwa Mskiti huo utakuwa na uwezo wa kutumiwa na Waumini zaidi ya Mia Tano (500) kwa wakati mmoja na Madrasa yenye Madarasa mawili yanayochukuwa wanafunzi Sitiini (60), Ofisi ya Imamu, Stoo, vyoo na Ofisi ya Mwalimu Mkuu.

Ujenzi wa Mskiti na Madrasa hiyo unatoka na maombi ya Wazee wa Kijiji cha Kisiwani kwa Bint Abeid kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya hali ya uchakavu wa Mskiti wa awali na kupelekea kuwakosesha Amani wakati wa Ibada.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR )

.Oktoba 16, 2026.

Post a Comment

0 Comments