6/recent/ticker-posts

Safari za Shirika la Ndege la Brussels Airlines kutoka Brussels - KIA zazinduliwa Rasmin

Tanzania imeandika historia mpya katika sekta ya usafiri wa anga na utalii baada ya Shirika la Ndege la Brussels Airlines kuzindua rasmi safari zake za moja kwa moja kati ya Brussels, Ubelgiji na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) katika hafla iliyofanyika Juni 3, 2026.

Kuanza kwa safari hizo ni utekelezaji wa Mkataba wa Huduma za Usafiri wa Anga kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ufalme wa Ubelgiji uliosainiwa Novemba 3, 2021 jijini Dodoma, ukilenga kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafiri wa anga, biashara, utalii na uwekezaji.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya ndege hiyo iliyowasili kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Millya (Mb), amesema uzinduzi wa safari hizo kutoka Brussels, makao makuu ya Umoja wa Ulaya (EU), ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Ubelgiji pamoja na nchi nyingine za Ulaya.

Mhe. Millya alieleza kuwa safari hizo zitafungua fursa mpya za kiuchumi kwa kurahisisha usafiri wa wageni, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ulaya kuja Tanzania, sambamba na kuwapa Watanzania urahisi zaidi wa kusafiri kwenda Ulaya kupitia mtandao mpana wa safari za Brussels Airlines.

Aidha, kuanzishwa kwa safari hizo kunatarajiwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya utalii nchini ikiwemo Zanzibar, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire. Hatua hiyo pia itasaidia kuongeza mapato yatokanayo na utalii, kuongeza ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.










Post a Comment

0 Comments